Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yahitaji ufadhili kuimarisha huduma za afya CAR

WHO yahitaji ufadhili kuimarisha huduma za afya CAR

Mfumo wa huduma za afya nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati umeathiriwa na migororo inayoendelea nchini humo, limesema leo shirika la Afya Duniani WHO, huku takwimu kuhusu afya ya umma zikizidi kuwa mbaya. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte

(Taarifa ya Priscilla)

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva Uswisi, msemaji wa WHO Tarik Jasarevic amesema kiwango cha vifo vya watoto kimekuwa miongoni mwa viwango vibaya zaidi duniani, huku watoto 139 kati ya 100,000 wakifariki duniani kabla ya kufikia umri wa miaka mitano.

(Sauti ya Bwana Jasarevic)

“Tunachoshuhudia kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita tangu kuanza kwa mgororo nchini Jamhuri ya Afrika ya Karti ni milipuko. kumekuwa na mlipuko wa surua, kichaa cha mbwa na kifaduro. Kuna hatari pia ya malaria na kipindupindu kwa watu wanaoishi kwenye mazingira magumu hasa wakati ambapo msimu wa mvua unaendelea.”

WHO imesema sekta ya afya bado inahitaji dola milioni 40 ili kutimiza mahitaji yake, wakati ambapo vituo vingi vya afya havifanyi kazi na nchi inakumbwa na ukosefu wa wahudumu wa afya.