Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha mkutano baina ya Korea Kusini, Japan na Uchina

Ban akaribisha mkutano baina ya Korea Kusini, Japan na Uchina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha mkutano uliofanyika mjini Seoul, hapo jana Novemba mosi baina ya Jamhuri ya Korea, Japan na Uchina.

Ban amewapongeza viongozi watatu walioshiriki mkutano huo, wakiwa na Waziri Mkuu wa Uchina, Li Keqiang, Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe na mwenyeji wao Rais Park Geun-hye wa Jamhuri ya Korea (Kusini) kwa kuanzisha tena mikutano hiyo ya nchi tatu katika kipindi cha miaka mitatu.

Taarifa ya msemaji wake imesema Katibu Mkuu ameeleza matumaini yake kuwa kuanza tena kwa mikutano hiyo kutaimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo tatu, na kuimarisha pia ushirikiano kaskazini mashariki mwa Asia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Umoja wa Mataifa unahimiza pande zote kufanya kazi pamoja ili kuendeleza kuaminiana na ushirikiano kwa ajili ya amani na ufanisi wa kikanda.