Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano kuhusu afya ya mama na mtoto laanza Mexico

Kongamano kuhusu afya ya mama na mtoto laanza Mexico

Kongamano la wataalam kuhusu afya ya mama na mtoto linafanyika katika mji mkuu wa Mexico Mexico City, likiwaleta pamoja watunga sera, watafiti, wataalam na wanaharakati zaidi ya 1,000 kutoka nchi 75. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Ukiwa ndio mkutano wa kwanza mkubwa kufanyika tangu kuzinduliwa kwa malengo ya maendeleo endelevu jijini New York wiki tatu zilizopita, kongamano hilo linatoa fursa kwa wadau katika masuala ya afya ya mama na watoto wachanga kuweka mikakati inayohitajika ili kutimiza malengo madogo yaliyomo katika ajenda ya maendeleo endelevu kuhusu afya ya akina mama, watoto na barubaru.

Kongamano hilo litajadili mikakati ya kuwezesha kumfikishia kila mama na kila mtoto mchanga huduma bora za afya, pamoja na mbinu za kutokomeza vifo vya akina mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, wanawake wengi zaidi na watoto wachanga sasa wananusurika vifo kuliko zamani kote duniani, lakini bado wanawake 800 na watoto wachanga zaidi ya elfu saba hufariki kila siku kutokana na matatizo ya mimba, uzazi na sababu nyingine zinazoweza kuzuiliwa. Aidha, zaidi ya watoto elfu saba hufariki tumboni mwa mama kila siku.