Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais Kenyatta asifu ajenda 2030, ataka maono ya pamoja kuifanikisha

Rais Kenyatta asifu ajenda 2030, ataka maono ya pamoja kuifanikisha

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, amesema tangu kupitshwa kwa malengo ya milenia mwongo mmoja na nusu, kumekuwepo na mafaniko mengi, japo changamoto sio haba.

Rais Kenyatta amesema hayo wakati wa hotuba yake kwa Baraza Kuu la Sabini la Umoja wa Mataifa.

Akitolea mfano maendeleo yaliyopatikana baada ya kupitishwa kwa malengo ya milenia, Rais Kenyatta amesema viwango vya mapato vya watu vimeongezeka huku idadi ya watu wanaoishi katika hali ya umaskini uliokithiri pamoja na vifo vya watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja imepungua maradufu.

Akipigia upato mafanikio nchini Kenya, Rais Kenyatta amesema..

(SAUTI KENYATTA )

“Nchini Kenya, tumefanya maendeleo makubwa katika muongo uliopita. Kwa mfano, tangu kupitishwa kwa elimu ya bure ya msingi kwa wote mwaka 2003, viwango vya waliojiunga na shule vimeongezeka kutoka asilimia 88 hadi asilimia 116. Na cha zaidi, tumefikia usawa wa kijinsia katika shule za msingi huku mpito kuanzia shule za msingi hadi sekondari na vyuo vikiboreshwa sana”

Licha ya mafanikio hayo chanya, Rais Kenyatta ameaonya kwamba kuna tofauti ya maendeleo kati ya mataifa mengi, sawa na hali usiokubalika ya juu ya umasikini vijijini.

Kwa maantiki hiyo, muarobaini ya kufanikiskwa kwa ajenda ya maendeleo endelevu, SDG’s, Rais Kenyatta amesema ni..

(SAUTI KENYATTA )

“Funzo kutoka utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ni kwamba sehemu kubwa inaweza kuafikiwa wakati dunia inapounganana na kumulika maono na malengo ya pamoja . Ajenda mpya tunayopitisha hii leo ni mpango kamambe kwa ajili ya hatua ya pamoja ya kubadilisha hatima ya binadamu , kwa kuinua watu wote kutoka umaskini, bila kuathiri uwepo wa sayari yetu."