Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa ni lazima tutumie SDGs kuubadilisha ulimwengu- Ban

Sasa ni lazima tutumie SDGs kuubadilisha ulimwengu- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema leo kuwa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) ni mwongozo katika safari ya kuelekea mustakhbali bora zaidi.

Ban amesema hayo akikutana na waandishi wa habari mjini New York, muda mfupi baada ya kupitishwa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na nchi wanachama. Akiitaja siku hii kama yenye kupewa uzito mkubwa, Ban amekumbusha ujumbe wa Papa Francis mapema asubuhi kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, akisisitiza wajibu wa kila mmoja wa kimaadili kuwasaidia watu masikini na kuitunza sayari dunia.

“Leo, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wameitikia changamoto hiyo kwa kupitisha Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu. Hii siyo ajenda ya mtu mwingine. Ni ahadi ya viongozi wa dunia kwa kila mtu. Malengo 17 ya maendeleo endelevu sasa yatatuongoza kwa njia salama na fanisi zaidi, na yenye usawa zaidi.”

Ban ameyataja malengo hayo kama ratiba ya mambo ya kufanya kwa ajili ya watu na sayari dunia, akiongeza kuwa sasa ni wakati wa kuyatumia kuubadilisha ulimwengu.

“Hatupaswi kumwacha mtu yeyote nyuma. Sisi ndicho kizazi cha kwanza kinachoweza kutokomeza umaskini, utofauti na kukosa haki. Na tunaweza kuwa kizazi cha mwisho kinachotishiwa na mabadiliko ya tabianchi”