Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

#UNGA inafanyika kukiwa na mkanganyiko na matumaini: Ban

#UNGA inafanyika kukiwa na mkanganyiko na matumaini: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mkutano wa 70 wa Baraza kuu la Umoja huo unafanyika wakati dunia iko katika kipindi mkanganyiko na matumaini.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo kabla ya kuanza kwa mikutano ya ngazi ya juu ya baraza hilo hapo wiki ijayo, Ban amesema ni mkanganyiko kwa kuwa mizozo inazidi kushika mizizi kila uchao raia wakigharimika zaidi na pia ni matumaini kwa kuwa viongozi wakuu wa nchi watakutana kusaka suluhu sambamba na kupitisha ajenda mpya ya maendeleo yenye matumaini.

Amegusia mizozo ya Syria, Sudan Kusini, Yemen na Libya akitaka pande husika zishirikiane kumaliza machungu huku akizungumzia sakata la wakimbizi wanaosaka hifadhi Ulaya akisema..

“Nawataka wale wanaozuia haki za wakimbizi wajiweke wao katika nafasi za wakimbizi hao. Watu wanaokabiliwa na mabomu na ukatili kwenye nchi zao wataendelea kusaka maisha kwingineko. Watu wenye matumaini finyu makwao wataendelea kusaka fursa kwingineko. Hii ni kawaida, ni jambo ambalo kila mmoja wetu angalijifanyia, hata kwa watoto wetu.”

Ban amesema kuwa majanga yanayotokea sasa ni kiashiria cha kushindwa kwa mfumo wa muda mrefu wa amani, ulinzi na maendeleo.

Alipoulizwa na waandishi wa habari maoni yake iwapo anaona huu ni wakati muafaka kwa mwanamke kushika wadhifa wa Katibu Mkuu baada ya yeye kuhitimisha kipindi chake mwakani, Ban amesema..

(Sauti ya Ban)

“Ingawa natambua kuwa kuna wanawake wengi viongozi wenye sifa, uzoefu na wanaojitoa kwa dhati, jukumu lote ni la nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuamua ni mtu gani atafaa zaidi kuongoza chombo hiki.”

Waandishi walipohoji dhima ya Umoja wa Mataifa wakati huu bado kuna mizozo, Ban amesema ni kweli kuna matatizo mengi kuliko suluhusho lakini bila Umoja wa Mataifa umwagaji damu ungalikuwa kiwango kikubwa zaidi kuliko sasa na anajivunia kuongoza chombo hicho.