Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na WFP zawasaidia maelfu waliokuwa hawafikiki kwa miezi kadhaa Sudan Kusini

UNICEF na WFP zawasaidia maelfu waliokuwa hawafikiki kwa miezi kadhaa Sudan Kusini

Licha ya hali tete ya kiusalama katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini, Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameweza kufikisha misaada ya chakula na lishe inayohitajika kwa dharura kwa makumi ya maelfu ya watu ambao walikuwa wametenganishwa na usaidizi wa kibinadamu kwa miezi kadhaa.

Mashirika hayo, yakiwa ni lile la Kuwasaidia watoto, UNICEF na lile la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, yamepeleka timu ya misaada ya dharura kuwasaidia zaidi ya watu 27,000 katika eneo la Wau Shilluk, kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Nile, ng’ambo ya mji wa Malakal.

Hii ni mara ya kwanza mashirika hayo kuweza kuwafikia watu walioko Wau Shilluk tangu mwezi Machi. Awali, matatizo ya usafiri na usalama yalikuwa yamezuia mashirika ya kibinadamu kuwafikia wati wanaoishi Wau Shilluk na maeneo mengine ya vijijini kwenye jimbo la Upper Nile.George Fominyen ni msemaji wa WFP nchini Sudan Kusini.

(Sauti ya George)

"Kilicho muhimu hapa ni kuwafikia watu wasio katika vituo vya ulinzi wa raia vinavyoendeshwa na ujumbe wa umoja wa mataifa, kwani wengi wanaokabiliwa na mzigo mkubwa wa mgogoro huu ni wale waliopo nje. Wako katika maeneo mengine, wanaishi katika vijiji na wanahifadhiwa na jamii, au wanajificha misituni, na msaada huu wa WFP na UNICEF utawafikia watu hawa."