Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Djinnit ataka vikosi hasimu viondoshwe ukanda wa Maziwa Makuu

Djinnit ataka vikosi hasimu viondoshwe ukanda wa Maziwa Makuu

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kwenye nchi za Maziwa Makuu, Said Djinnit, amekariri haja ya kuviondosha vikosi vyote hasimu kwenye ukanda wa Maziwa Makuu, likiwemo kundi la FDLR, akiahidi kuwa tayari kufanya kazi kwa karibu na wadau wa kikanda na wa kimataifa, ili kuongeza kasi ya juhudi za kuviondosha vikundi hasimu.

Kwa mantiki hiyo, Bwana Djinit amesisitiza haja ya kuanzisha tena mapema ushirikiano wa kijeshi baina ya MONUSCO na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, katika operesheni dhidi ya FDLR.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ambaye amekuwa ziarani mjini Kigali, Rwanda kuanzia tarehe 19 hadi 22 Agosti, ametoa pia wito wa kuharakisha shughuli ya kuwarejesha askari wa zamani, kama ilivyoamriwa na viongozi wa kikanda katika mkutano wao wa mwisho mjini Luanda, Angola.

Ziara ya Bwana Djinit nchini Rwanda ni sehemu ya mashauriano yake na nchi zilizosaini mkakati wa amani, usalama na ushirikiano kwa ajili ya DRC na ukanda mzima.