Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania miongoni mwa nchi 9 kushuhudia ukuaji mkubwa wa idadi ya watu

Tanzania miongoni mwa nchi 9 kushuhudia ukuaji mkubwa wa idadi ya watu

Katika ripoti kuhusu idadi ya watu duniani iliyotolewa leo, Umoja wa Mataifa unatarajia kuwa nusu ya ukuaji wa watu duniani utatokea kwenye nchi 9 zenye kiwango cha juu cha uwezo wa kuzaa duniani, Tanzania ikiwa moja wazo.

Nchi zingine zitakazochangia pakubwa kwenye ukuaji wa idadi ya watu ifikapo mwaka 2050 ni India, Nigeria, Pakistan, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo DRC, Ethiopia, Marekani (USA), Indonesia na Uganda.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya watu duniani imefika bilioni 7.3 mwaka huu, ikitarajia kufika bilioni 9.7 mwaka 2050.

John Wilmoth, Mkurugenzi wa Kitengo cha Idadi ya Watu kwenye Idara ya Maswala ya Kijamii na Kiuchumi DESA ya Umoja wa Mataifa, anaeleza kuwa ukuaji wa idadi ya watu ni mkubwa zaidi barani Afrika kwani bado kila mwanamke anazaa takriban watoto 4.7.

“ Jamii yenye kiwango cha juu cha uwezo inakuwa kwa kasi, vijana na watoto wakiwa wengi. Na hiyo ni changomoto kwa upande wa kukuza mifumo ya elimu na afya na kuwahudumia vijana hawa ili wachangie kwenye ukuaji wa uchumi wa jamiii zao.”