Watalaam wa Umoja wa Mataifa waonya Jamhuri ya Dominika kuhusu kufukuza watu

Watalaam wa Umoja wa Mataifa waonya Jamhuri ya Dominika kuhusu kufukuza watu

Watalaam wa Umoja wa Mataifa leo wameiomba serikali ya Jamhuri ya Dominika kuchukua hatua ili kuzuia uhamisho kiholela wa watu wenye asili ya Haiti.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya watu wenye asili ya kiafrika, Mireille Fanon Mendes-France, amesema hakuna mtu yeyote anayepaswa kufukuzwa nchini Jamhuri ya Dominika akiwa na haki ya kuishi nchini humo.

Tayari karibu watu 19,000 wameshahamia Haiti wakiwa na hofu ya kunyanyaswa wakati ambapo uhamisho unatarajiwa kuanzia rasmi mwezi Agosti mwaka huu.

Bi Fanon Mendes-France ameeleza kwamba watu wenye asili ya Haiti waliozaliwa Jamhuri ya Dominika wanakumbwa na changamoto kadhaa wakijaribu kupata vitambulisho, huku wakishindwa kupata taarifa kamili kutoka kwa serikali kuhusu mpango huo wa uhamisho.

Halikadhalika ameisihi serikali ya Jamhuri ya Dominika kuunda sera na mikakati ili kupambana na unyanyasaji na ubaguzi dhidi ya watu hao.

Maelfu ya watu waliozaliwa Jamhuri ya Dominika wenye asili ya Haiti wameshindwa kupata vitambulisho kufuatia sheria mpya iliyopitishwa nchini humo mwaka 2014, huku serikali ikipanga kuwahamishia Haiti watu hao wasiokuwa na uraia.