Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii ya kimataifa yapaswa kuheshimu haki za binadamu wakati wa kupambana na ugaidi: Ban

Jamii ya kimataifa yapaswa kuheshimu haki za binadamu wakati wa kupambana na ugaidi: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ongezeko la idadi ya watu wanaovuka mipaka ili kujiunga na vikundi vya kigaidi ni dalili ya ongezeko la itikadi kali duniani kote, na hatua zinapaswa kuchukuliwa na jamii ya kimataifa ili kukabili changamoto hilo.

Bwana Ban amesema hayo kwenye ujumbe uliotolewa kwa njia ya video kwa ajili ya mkutano maalum unaofanyika mjini Madrid kuhusu swala hilo, ukiandaliwa na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na ugaidi, CTED.

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba licha ya hatua za kiusalama na kijeshi ambazo zinapaswa kuchukuliwa, jibu la jamii ya kimataifa linapaswa kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

Amesema jitihada za kupambana na ugaidi zinazokiuka haki za binadamu zinasaliti maadili ya jitihada hizo na kuchochea zaidi itikadi kali.

Hatimaye ameeleza kwamba anaanda mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia itikadi kali unaotarajiwa kupelekwa mbele ya Baraza la Usalama kabla ya mwisho wa mwaka huu.