Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Somalia

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na kikao cha mashauriano kuhusu Ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Maman Sidikou, Mwakilishi Maalum wa Kamisheni ya AU ambaye pia ni Mkuu wa AMISOM, Nicholas Kay, Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Somalia, UNSMOM na Waziri Mkuu wa Somalia, Omar Abdirashid Ali Sharmarke, ambao wamekutana na waandishi wa habari mara tu baada ya kikao.

Katika mkutano na wanahabari, Mkuu wa UNSOM, Nicholas Kay amesema Somalia bado inamulikwa kwenye ajenda ya Baraza la Usalama kwa sababu bado inakabiliwa na matatizo na changamoto za kisiasa, umaskini, na machafuko. Licha ya hayo, amesema kuna matumaini, kwani nchi hiyo imeanza kujikwamua tena baada ya miongo ya mkwamo na migogoro, huku akieleza ni kwa nini ufanisi huo unapatikana..

“Kwanza, ni kwa sababu ni mchakato wa kisiasa ambao kimsingi unamilikiwa na kuongozwa na Wasomali wenyewe, na pili, ni kwa sababu ya ubia wa aina yake baina ya Muungano wa Afrika, Umoja wa Mataifa, serikali ya Somalia na Muungano wa Nchi za Ulaya, EU, na tatu, imekuwa na ufanisi kwa sababu ya operesheni za kijeshi, na sehemu hiyo ya kijeshi ndiyo ambayo tumekuwa tukiangazia na Baraza la Usalama, kuona jinsi ya kuimarisha operesheni za AMISOM hata zaidi katika hii awamu ya mwisho hadi mwaka 2016, yatakapohitimishwa mamlaka ya serikali ya sasa na bunge.”

Naye Mkuu wa AMISOM, Maman Sidikou ameeleza umuhimu wa kuimarisha AMISOM na kuerejesha utulivu Somalia..

“Somalia ndipo ufanisi unapohitajika, iwapo hatutaki kuuacha ukanda mzima utumbukie katika machafuko kama kanda zingine. Zoezi la kutathmini uwezo wa AMISOM sasa pia linahusu kufanyia marekebisho na kuiimarisha AMISOM, ili iweze kuhimili kile Al-Shabaab inajaribu kututendea, ambavyo ni vita vya kupiga na kutoroka, na kutuwezesha kuwaandama kwa njia tunayopaswa kuwaandama, na kuwamaliza kabisa, kwani hiyo tu ndiyo lugha wanayoijua.”

Waziri Mkuu wa Somalia Ali Sharmarke amesema Somalia imetoka mbali sasa, na wana ndoto ya kuona Somalia ikiwa nchi ambayo imeungana hapo mwakani, ikiwa haina mitandao ya kigaidi, na ikifungua milango yake ya uwekezaji kwa ulimwengu.