Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waadhimisha miaka 20 ya mkutano wa dunia wa maendeleo ya jamii

Umoja wa Mataifa waadhimisha miaka 20 ya mkutano wa dunia wa maendeleo ya jamii

Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa limekutana leo kwa ajili ya mkutano maalum wa maadhimisho ya miaka 20 tangu mkutano wa dunia kuhusu maendeleo ya jamii huko Copenhagen, Denmark. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Mkutano huo unafanyika wakati wa kikao cha uongozi wa ECOSOC, huku Umoja wa Mataifa ukitarajia kupitisha malengo mapya ya maendeleo endelevu mwezi Septemba mwaka huu.

Akiongea kwenye uzinduzi wa mkutano huu, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson ameeleza umuhimu wa maendeleo ya jamii duniani.

(sauti ya Eliasson)

"Malengo yameamuliwa Copenhagen mwaka 95 baada ya miongo ya utafiti kuhusu namna ya kuunganisha kwa ufanisi maendeleo kwa upande wa kijamii, kimazingira na kiuchumi ili kuhakikisha si tu ukuaji endelevu wa uchumi lakini pia utu kwa wote. Kutokomeza umaskini, mshikamano wa jamii na ajira  bado ni mahitaji ya msingi ili watu waishi maisha yao kwa usalama na utu, na haki zao ziheshimiwe."

Azimio lililopitishwa wakati wa mkutano wa Copenhagen mwaka 1995 lilisisitiza uhusiano kati ya ukuaji endelevu wa uchumi, mshikamano wa jamii na ajira kwa wote na kuzingatia umuhimu wa kuzingatia binadamu katika mipango yote ya maendeleo.