Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaonya kuhusu athari za tumbaku haramu

WHO yaonya kuhusu athari za tumbaku haramu

Wataalam wa afya wameonya leo kuhusu athari za biashara haramu ya tumbaku, kiafya, kiuchumi na kiusalama, wakisema kuwa huenda sigara moja kati ya kila kumi zinazovutwa duniani imetokana na biashara hiyo. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

Taarifa ya Assumpta

Onyo hilo limekuja siku chache kabla ya Siku ya Tumbaku Duniani, ambayo ni Mei 31. WHO imetoa wito kwa nchi zaidi zikabiliane na biashara haramu katika tumbaku, kwa kusaini mkataba mpya unaopiga marufuku biashara hiyo. Katika mahojiano na Redio ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Vera Luiza da Costa e Silva ameelezea baadhi ya madhara ya biashara hiyo..

“Biashara haramu ya tumbaku inaongeza matumizi, na ongezeko la matumizi linaleta maradhi yatokanayo na tumbaku, na hiyo inazidisha ongezeko la bei ya tiba, na huo ni mzigo mara mbili kwa serikali. Mkataba wa kupiga marufuku biashara haramu ya tumbaku ndio suluhu pekee ya kuondoa tatizo hili, kwa hivyo sekta zote mbali na sekta ya afya, ni lazima zishiriki katika mchakato huu, na serikali lazima ziuunge mkono.”

Iwapo mkataba huo utasainiwa na nchi 40, basi utakuwa sheria. Kufikia sasa, umesainiwa na nchi 8 pekee. Hata hivyo, WHO imesema kuwa mkataba huo unakabiliwa na pingamizi kubwa kutoka kwa sekta ya tumbaku.