Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali bado ni mbaya kwa manusura wa tetemeko la ardhi Nepal- UNFPA

Hali bado ni mbaya kwa manusura wa tetemeko la ardhi Nepal- UNFPA

Shirika la Mfuko wa Idadi ya Watu, UNFPA, limesema leo kuwa hali bado ni tete kwa manusura wa tetemeko la ardhi la Aprili 25 nchini Nepal.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNFPA, bado taifa hilo linaathiriwa na madhara ya tetemeko hilo, na kwamba tetemeko lililofuata mnamo Mei 12, liliongeza idadi ya vifo kwa idadi kubwa ilosababishwa tayari na janga hilo.

UNFPA imesema kwamba wakati msimu wa mvua unapokaribia kuanza wiki chache zijazo, huenda hali ya manusura hao ikazorota zaidi, wakati wengi wao wakiwa tayari hawahisi salama kuwa ndani ya nyumba kwa sababu ya kuendelea zogo chini ya ardhi.

Mvua hiyo pia inatarajiwa kuongeza maporomoko ya udongo, na kupunguza uwezo wa kuvifikia vijiji vilivyoathiriwa.

UNFPA inajitahidi kuwafikia manusura katika vijiji vilivyoathiriwa zaidi, na kutoa vifaa vya kusaidia katika uzazi, huduma za uzazi salama na mikoba yenye vifaa vya kujisafi.