Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tiba dhidi ya magonjwa hatarini yaendelea Nepal: WHO

Tiba dhidi ya magonjwa hatarini yaendelea Nepal: WHO

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema tiba dhidi ya magonjwa hatari kama vile kifua kikuu, kisukari na kiharusi zimeendelea nchini Nepal hata baada ya tetemekeo kubwa la ardhi lililokumba nchini mwishoni mwa mwezi uliopita.

Mkuu wa waganga na mifumo ya afya WHO Dkt. Frank Paulin amesema licha ya maeneo mengine kukumbwa na mkwamo, matibabu yameendelea kwa kuzingatia kuwa ukosefu wa tiba kama vile kifua kikuu unaweza kuwa chanzo cha maambukizi kwa wengine.

Dkt. Paulin amesema hatua hiyo imewezekana kutokana na kuwepo kwa mipango ya awali iliyowezesha kuendelea utoaji wa dawa kwenye maeneo kama vile hospitali ya Alka inayotibu wagonjwa wa kifua kikuu iliyoko kusini mwa mji mkuu Kathmandu.

Mmoja wa watoa tiba kwenye hospitali hiyo amesema mwitikio wa wagonjwa kuchukua dawa hata baada ya tetemeko umetokana na kuhamasika na kutambua kuwa kukosa hata dozi moja dhidi ya kifua Kikuu kunaweza kudhoofisha matibabu kamili.