Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMA yalaani shambulio la Taliban dhidi ya majaji na waendesha mashitaka:

UNAMA yalaani shambulio la Taliban dhidi ya majaji na waendesha mashitaka:

Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Usaidizi nchini Afghanistan (UNAMA) umelaani vikali shambulio la kujitoa muhanga la jana Jumapili dhidi ya basi la raia lililokuwa likisafirisha wafanyakazi wa ofisi ya mwanasheria mkuu mjini Kabul.

Kundi la Taliban limedai kuhusika na shambulio hilo lililokatili maisha ya waendesha mashitaka watano wakiwemo wanawake watatu na kujeruhi raia wengine 19.

Naibu mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini Afghanistan Tadamichi Yamamoto amesema vitendo vya makusudi dhidi ya raia ambao ni wafanyakazi wa ofisi ya mwanasheria mkuu na wataalamu wengine wa sheria ni vitendo visivyokubalika na ni lazima vikomeshwe.

Ameongeza kuwa mashambulizi hayo ya makusudi yanayowalenga raia pia yanakwenda kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu na yanachukuliwa kama ni uhalifu wa vita.

Tangu Januari mosi hadi tarehe 10 May 2015, kundi la Taliban kupitia tovuti yake imedai kuhusika na mashambulio 11 dhidi ya wataalamu wa sheria na mahakama,  mashambulio ambayo yamesababisha maafa kwa watu 114, 28 wamefariki dunia na 86 kujeruhiwa.