Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yafanya mkutano na wahisani kuhusu watu wanaorejea makwao Pakistan

OCHA yafanya mkutano na wahisani kuhusu watu wanaorejea makwao Pakistan

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA imeitisha mkutano wa wahisani wa misaada ya kibinadamu ili kuwapa jumuiya ya wahisani wa kimataifa taarifa kuhusu hali ya jumla ya majimbo ya Khyber Pakhtunkwa na maeneo ya kikabila yanayodhibitiwa na serikali nchini Pakistan.

Wahisani wamepewa tathimini ya mchakato wa watu wanaorejea nyumbani na mahitaji yao. Watu walianza kurejea mwezi Machi mwaka huu kusini mwa Waziristan, Kaskazini mwa Waziristan na viunga vya Khyber .

Kwa mujibu wa OCHA hadi sasa watu 98,000 wamesharejea nyumbani baada ya kutawanywa kwa miaka mingi.

Januari mwaka huu OCHA na timu yake nchini Pakistan ilitoa mpango wa kusaidia mahitaji ya wakimbizi wa ndani na wanaorejea makwao. Mpango huo unalenga kukusanya dola milioni 433 na mpaka sasa ni dola milioni 290 tu ndio zilizokusanywa huku serikali ikichangia dola milioni 60 zilizotokana na ngano kupitia shirika la mpango wa chakula duniani WFP.