Rais Kikwete kuhutubia kuhusu masuala ya ajira New York

27 Machi 2015

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete atashiriki kwenye mkutano maalum utakaofanyika mjini New York wiki ijayo kuhusu mikakati mipya ili kufikia maendeleo endelevu pamoja na kutokomeza ukosefu wa ajira.

Rais Kikwete atahutubia mkutano huo utakaoanza tarehe 30 Machi hadi Mosi Aprili, mkutano ambao umeandaliwa na Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC na Shirika la Kazi Duniani ILO.

Wengine watakaohutubia ni Mawaziri wakuu wa Sweden na Bahama na washindi wa tuzo ya Nobel na wataalam wa uchumi Dkt. Joseph Stiglitz na Robert Shiller.

Akimulika umuhimu wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Rider amesema ajira bora inayolenga watu zaidi na kuwawezesha kiuchumi na kijamii ni msingi wa maendeleo endelevu.

Kwa sasa, watu milioni 202 hawana ajira duniani kote, na wengine mamilioni wanafanya kazi kwenye hali ya kuteseka, ambapo mfanyakazi mmoja kati ya watatu anaishi kwa chini ya dola mbili kwa siku.

Maswala yatakayojadiliwa pia ni fursa ya kubuni ajira zinazosaidia kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, pamoja na umuhimu wa kukabiliana na changamoto zinazokumba wanawake na vijana katika ajira.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter