Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais mteule wa kikao cha 69 cha Baraza Kuu atangaza maudhui ya mkutano

UN Photo/Eskinder Debebe)
Rais mteule wa mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Sam Kutesa kutoka Uganda akihutubia baraza baada ya uteuzi. (@

Rais mteule wa kikao cha 69 cha Baraza Kuu atangaza maudhui ya mkutano

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha 93 cha wazi na ajenda kuu ni uteuzi wa Rais wa mkutano wa 69 utakaoanza tarehe 16 Septemba mwaka huu..

Rais wa Baraza hilo kwa sasa John Ashe alieleza wajumbe kuwa Bara la Afrika ambalo kwa mujibu wa kanuni ndilo linalopaswa kuchukua wadhifa limewasilisha jina pekee la Sam Kutesa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda kushika nafasi hiyo…na kwa mujibu wa Kanuni za Baraza akatangaza…

Anasema kwa mantiki hiyo namtangaza Mheshimiwa Sam Kutesa wa Jamhuri  yaUgandakuwa amechaguliwa bila kupingwa…..

Ndipo Rais huyo mteule wa Baraza akapatiwa fursa ya kuzungumza, akitanguliza shukrani na kueleza kuwa sasa kuna changamoto kubwa zinazokabili dunia lakini kwa pamoja nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinaweza kushirikiana na kukabiliana nazo.

Amesema umoja huo ndio umefanya chombo hicho kuendelea kuwa na umuhimu akitaja malengo ya maendeleo ya Milenia yanavyochochea mabadiliko.

Bwana Kutesa akapendekeza maudhui ya mkutano wa 69 ambayo ni Kufanikisha na kutekeleza ajenda ya mabadiliko baada ya mwaka 2015 ambapo amesema...

(Sauti ya Kutesa)

Maudhui haya yanapata msingi wa mafanikio muhimu yaliyopatikana kwenye mkutano wa sasa. Inasisitiza umuhimu wa siyo tu kujikita kwenye kuandaa au kukubaliana kuhusu ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, bali pia muhimu zaidi ni kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi.”

Mara baada ya uteuzi Katibu Mkuu Ban Ki-Moon na Rais wa Baraza Kuu John Ashe wamepongeza uteuzi wake wakisema wana matumaini makubwa kwa jukumu alilopatiwa ikiwemo ajenda baada ya mwaka 2015.

Pamoja na kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kuanzia 2005 hadi sasa, Kutesa ameshika nyadhifa  nyingine ikiwemo waziri wa Nchi akihusika na fedha, na mipango pamoja na mwanasheria mkuu wa serikali mwaka 1996-2000.