Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utafiti waonyesha ukatili dhidi ya watoto Malawi umeenea- UNICEF

Utafiti waonyesha ukatili dhidi ya watoto Malawi umeenea- UNICEF

Watu wawili kati ya watatu nchini Malawi hukumbana na ukatili wakiwa watoto, huku msichana mmoja kati ya watano akikumbana na ukatili wa kingono kabla ya kutimu umri wa miaka 18, limesema Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Hayo yamebainika katika ripoti mpya ya utafiti uliofanywa nchini Malawi kuhusu ukatili dhidi ya watoto na wasichana, ambayo itazinduliwa hapo kesho.

Mbali na wasichana, wavulana wawili kati ya kila watatu pia hukumbana na ukatili wa kimwili kabla ya kutimu umri wa miaka 18.

Utafiti huo ambao ndio wa kwanza kuchunguza tatizo la ukatili dhidi ya watoto kote nchini Malawi, uliangazia ukatili wa kingono, kimwili na kihisia. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukatili dhidi ya watoto umekuwa jambo la kawaida katika jamii nyingi kote nchini Malawi.

Utafiti huo uliofadhiliwa na DFID, ulifanywa na Wizara ya Jinsia, Watoto, Ulemavu na Huduma za Kijamii, Kituo cha Utafiti wa Kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Malawi, Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF na Vituo vya Marekani vya Kudhibiti Magonjwa, CDCC, na ulimulika watu wenye umri kati ya miaka 18-24, na miaka 13-17.