Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lakariri nia yake ya kuiwekea Sudan Kusini vikwazo

Baraza la usalama lakariri nia yake ya kuiwekea Sudan Kusini vikwazo

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamesema kuwa hali nchini Sudan Kusini inahitaji kukabiliwa kwa dharura, wakiongeza kuwa pande zote zinazozozana zinapaswa kutoa amri dhahiri zinazopinga ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria ya haki za binadamu, na ukiukwaji mwingine bila kuchelewa.

Baraza hilo limeelezea kusikitishwa na kushindwa kwa Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar na pande zote kuafikia makubaliano kuhusu utaratibu wa mpito uliopendekezwa mnamo Februari 1 2015 kuhusu kuwekwa kwa serikali ya mpito kufikia Machi 5 2015.

Taarifa ya wanachama wa Baraza la Usalama imesomwa na Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Machi, Mwakilishi wa Ufaransa Francois Delattre ..

“Baraza la Usalama linarudia kulaani vikali ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha uhasama, yaliyosainiwa na Jamhuri ya Sudan Kusini na SPLM/A Upinzani mnamo Januari 23 2014, na linasisitiza kuwa vitendo vya Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani wanapoendelea kuandama suluhu la kijeshi kwa mzozo huu, vinakwenda kinyume na wajibu wao chini ya makubaliano ya kusitisha uhasama.”

Baraza hilo limekariri nia yake ya kuweka vikwazo vyovyote stahiki, ambavyo huenda vikajumuisha kuzuia uuzaji na usafirishaji wa silaha na vikwazo vya usafiri kwa maafisa wa ngazi ya juu wanaowajibika kwa vitendo na sera zinazohatarisha amani, usalama na ustawi wa Sudan Kusini, ili kuishawishi serikali na makundi ya upinzani kuunda serikali ya pamoja ya mpito.

Mwakilishi wa Sudan Kusini kwenye Umoja wa Mataifa Francis Deng, ameitikia taarifa hiyo kwa kusema..

“Acha nielezee kusikitishwa kwa ujumbe wangu kuwa Baraza hili linaendelea kujadilia masuala muhimu ya amani na usalama Sudan Kusini, bila kufanya mashauriano ya kina na Muungano wa Afrika. Hili halioani na moyo wa ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika, na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.”