Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la Sendai laafikia mfumo wa kupunguza hatari za majanga

Kongamano la Sendai laafikia mfumo wa kupunguza hatari za majanga

Kongamano la kimataifa kuhusu kupunguza hatari za majanga limehitimishwa leo mjini Sendai, Japan kwa kuafikia mfumo wa udhibiti wa majanga, wa mwaka 2015 hadi 2030.

Mfumo huo unafuatia ule wa Hyogo wa kuchukua hatua, ulioafikiwa miaka kumi iliyopita, na ambao uliweka kwa kifupi mambo ya kipaumbele katika kujenga uwezo wa taasisi, serikali na mashirika kupunguza hatari za majanga. Mkakati wa Hyogo ulijikita pia katika kuendeleza uelewa wa watu kuhusu siyo tu majanga, bali pia hatari.

Katika mahojiano na Redio ya Umoja wa Mataifa, Margareta Wahlström ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu kupunguza hatari za majanga, amesema kilichofikiwa Sendai ni mkusanyiko wa uzoefu utokanao na hatua za kudhibiti hatari za majanga muongo mmoja uliopita, akiongeza kuwa anatumai mfumo huo utakuwa ishara muhimu mno..

“Unaweza kusema mfumo wa kupunguza hatari za majanga ni daraja kati ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu, kwa sababu unatoa mwelekeo wa hatua tekelezi. Ni muhimu kwa hatua nyingi za kujenga uthabiti, na bila kupunguza hatari za majanga, uendelevu wa maendeleo hauwezi kuwepo kwani, hauna kinga dhidi ya majanga yanayovuruga tegemeo la watu masikini kuishi na pia uwezo wa nchi tajiri kuendeleza kasi ya maendeleo ya kiuchumi.”

Bi Wahlström amesema mfumo huo wa Sendai ni hatua muhimu kuelekea mbele kuhusu jinsi ya kudhibiti hatari kwa uthabiti na maendeleo endelevu.