Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNISFA yakabiliana na wavamizi wa Misseriya waliowaua raia Abyei

UNISFA yakabiliana na wavamizi wa Misseriya waliowaua raia Abyei

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda usalama kwenye eneo la Abyei, mpakani kati ya Sudan na Sudan Kusini, UNISFA, umeripoti kuwa watu 100 waliojihami kutoka jamii ya Misseriya wamekivamia kijiji cha Marial Achak kusini mwa Abyei hii leo, na kuwaua watu 3 wa kabila la Dinka, kuwajeruhi 3 wengine na kuwateka nyara watoto 8.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema ujumbe wa UNISFA umesema nyumba 24 ziliteketezwa katika operesheni hiyo..

“Ujumbe huo umeanza kufanya doria kukabiliana na wavamizi hao, ambao ulikutana nao karibu na mji wa Jagak. Katika makabiliano ya mtutu wa bunduki, wapiganaji wanne wa Misseriya walikamatwa na watatu kuuawa. Walinda doria wa UNISFA pia waliwakabiliana na wanaume wanne wa Misseriya wasio na silaha wakiondoka kwenye eneo la tukio.”

Bwana Dujarric amesema operesheni hiyo inaendelea.

“Ujumbe wa UNISFA umesema hili ni tukio la nne baya mno kati ya jamii za Misseriya na Dinka katika miezi miwili iliyopita, ikiashiria mwelekeo wa kutia hofu wa kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama kwenye eneo hilo.”