Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSMA yakaribisha kuridhiwa kwa nakala ya makubaliano ya amani Mali

MINUSMA yakaribisha kuridhiwa kwa nakala ya makubaliano ya amani Mali

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, umepongeza pande husika kwa kuridhia nakala ya makubaliano ya amani na maridhiano hapo jana mjini Algiers, ambako kulifanywa na serikali ya Mali, na kundi moja kutoka muungano wa makundi yenye silaha, na wanachama wote wa upatanishi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema, MINUSMA inaelewa kuwa uratibu wa muungano wa makundi yenye silaha bado haujaridhia nakala hiyo, na umeomba muda wa ziada ili ufanye mashauriano na wafuasi wake nchini Mali.

“Ujumbe huo unasema kuwa nakala ya makubaliano ya amani ndio mwelekeo unaofaa zaidi kwa kukabiliana na changamoto nyingi zinazoikabili Mali, na imesema pia kuwa uungwaji mkono wa pamoja na endelevu kutoka jamii ya kimataifa unahitajika ili kuzisaidia pande husika kuhitimisha na kutekeleza mkataba jumuishi na endelevu wa amani”

Kwa mujibu wa Bwana Dujarric, MINUSMA imesema kuwajibika na kujitoa kwa pande husika za watu wa Mali ni muhimu kwa mafanikio, na imetoa wito kwa pande zote kuendelea kufanya mazungumzo kwa njia ya kujenga hadi kufikia makubaliano ya mwisho.