Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vurugu ya Nigeria yatandaa Niger: WFP

Vurugu ya Nigeria yatandaa Niger: WFP

Tunaanzia Afrika, Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limeelezea wasiwasi wake kuhusu vurugu inayozidi kaskazini mwa Nigeria na ambayo imeanza kutandaa katika maeneo ya Kusini Mashariki mwa  Niger.  Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Msemaji wa WFP Elisabeth Byrs amesema Niger ni nchi ya kwanza inayopokea wakimbizi wengi kutoka Nigeria, akiongeza kwamba mtoto mmoja mkimbizi kati ya kila watatu ameathirika na utapiamlo.

Licha ya hayo amesema jamii inayoishi katika maeneo hayo ya Niger tayari imekumbwa na tatizo la njaa.

(Sauti ya Byrs)

“  Tuna wasiwasi kuhusu wakimbizi lakini pia jamii zinazowapokea na familia zilizopo kwenye maeneo hayo, kwa sababu wakimbizi wametawanyka katika zaidi ya vijiji na maeneo 140. Na kwenye eneo hilo, raia wamekumbwa na ukame kwa miaka kadhaa, ndio maana matokeo ya ukame na idadi ya wakimbizi ni mzigo mzito kwa jamii kwenye eneo hilo, ndio maana tuna wasiwasi sana”  

Idadi ya kutoka Nigeria imefika 100,000 nchini Niger, na WFP inalenga kusaidia watu 130,000 nchini Niger pekee yake mwaka huu.