Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita dhidi ya ugaidi vitekelezwe kimataifa: Taubira

Vita dhidi ya ugaidi vitekelezwe kimataifa: Taubira

Baada ya kukumbwa na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya gazeti la Charlie Hebdo, Ufaransa imeamua kuchukua hatua ili kupambana na ugaidi, bila kuathiri haki za binadamu na demokrasia.

Christina Taubira ambaye ni waziri wa sheria wa Ufaransa amesema mkakati ulioamuliwa na Ufaransa ni tofauti na mikakati ya nchi nyingine ambazo zimezuia uhuru wa raia wake baada ya kukumbwa na ugaidi.

Alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York baada ya mkutano wa kamati ya makabiliano dhidi ya ugaidi uliofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Taubira amesema ingalikuwa rahisi kuanza kufuatilia kila mtu na kuzuia uhuru wa raia ili kudhibiti ugaidi, lakini Ufaransa haikutaka kufuata njia hiyo, kwa sababu ingaliweza kuathiri demokrasia.

Waziri huyo amesema suluhu kwa tatizo la ugaidi ni kwa ngazi ya kimataifa, ili kupata amani endelevu, kupitia faraja ya kila mtu na usawa baina raia.

Aidha ameongeza kwanza ni muhimu kupambana na sababu za msingi za ugaidi ikiwemo ukosefu wa usawa katika uchumi na elimu.