Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola bado ni tishio kubwa: Nabarro

Ebola bado ni tishio kubwa: Nabarro

Ugonjwa wa Ebola bado ni tishio kubwa, wameonya watalaam wa Umoja wa Mataifa wakisema mazishi yasiyozingatia kanuni za afya yamesababisha ongezeko la idadi ya maambukizi mapya.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, David Nabarro, amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana, maambukizi mapya yanaendelea kwa sababu watu wanakiuka kanuni za mazishi salama.

“ Njia ya kawaida zaidi ya kuambukizwa na Ebola ni kupitia matambiko yanayofanyika wakati maiti anazikwa, hasa kuiosha na kuigusa”

Dkt. Nabarro amesema hatari bado ipo, wakati idadi ya visa vipya vimeongezeka katika nchi tatu zilizoathirika na mlipuko huo, Liberia, Guinea and Sierra Leone.

Kwa upande wake, mtalaam wa Ebola katika Shirika la Afya Duniani, Bruce Aylward amesema ni muhimu sana kuzingatia ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu na wagonjwa kwani mlipuko unaendelea kusambazwa na watu hao wakisafiri kwa ajili ya biashara zao.

Hata hivyo ameongeza kwamba changamoto ni upungufu wa ufadhili, akitarajia fedha kumalizika mwisho wa mwezi huu tu, na dola bilioni moja bado ikihitajika. Amesema changamoto nyingine ni msimu wa mvua unaokaribia ambao amesema unaoweza kuathiri bidii za kutokomeza Ebola.