Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya Libya yarejeshwa nyumbani

Mazungumzo ya Libya yarejeshwa nyumbani

Washiriki wa mazungumzo ya kisiasa kuhusu Libya ambayo yamekuwa yakifanyika mjini Geneva wiki hii, wamekubaliana kuyahamishia mazungumzo ya siku zijazo nchini Libya, iwapo viwezesha shughuli na usalama utahakikishwa.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, umetoa wito kwa wadau wote kujiunga kwenye mazungumzo hayo yanayohisaniwa na Umoja wa Mataifa kwa njia ya uwazi na moyo wa kujenga.

Washiriki walielezea hofu yao kuhusu hali ya usalama katika maeneo tofauti, wakilaani hasa shambulizi la hivi karibuni mjini Tripoli, ambalo lilifanyika wakati wakikutana kwenye Ofisi ya Umoja wa Mataifa Geneva.

Wakati huo huo, wamesisitiza kuwa mazungumzo hayo yanatoa kipindi cha matumaini na maridhiano kwa watu wa Libya, na fursa ya kuyatatua matatizo ya kisiasa na kiusalama nchini mwao, ambayo haipaswi kupotezwa. Wameiomba UNSMIL kuanza mashauriano na wadau kuhusu mahali pa kufanyia mazungumzo ya siku zijazo.