Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi 800,000 Afrika wakabiliwa na uhaba wa chakula

Wakimbizi 800,000 Afrika wakabiliwa na uhaba wa chakula

Takriban wakimbizi milioni moja barani Afrika wanakabiliwa na uhaba wa chakula kwa viwango vya kutia hofu, huku mashirika ya Umoja wa Mataifa yakihangaika kukidhi mahitaji ya chakula yanayozidi kuongezeka.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR na lile la Chakula Duniani, WFP, yameanza kupunguza kiasi cha chakula kinachotolewa kwa wakimbizi, hali ambayo yamesema ni hatarishi, hususan kwa watoto wakimbizi, wengi wao ambao tayari wana utapiamlo wa viwango visivyokubalika, kudumaa na ukosefu wa damu.

Mashirika hayo sasa yanaomba dola milioni 225 ili kuyawezesha kurejelea utoaji wa chakula kwa kiasi kinachotosha na kuzuia kupunguzwa kwa posho zaidi katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Antonio Guterres ni Kamishna Mkuu wa UNHCR

“Siyo kwamba wafadhili wamekuwa wakisahau UNHCR au WFP. Ukweli ni kwamba, kuongezeka kwa migogoro ambako tunashuhudia mwaka 2014, pamoja na kwamba Afrika ni bara ambalo kwa njia moja limesahaulika, wakati dunia ikiangazia Syria, Ukraine na sasa Iraq, kumeweka hali ambayo imewafanya wakimbizi barani Afrika kukabiliwa na tatizo la chakula, na tatizo hili la uhaba wa chakula linahitajika kushughulikiwa, na njia ya kulishughulikia ni kutoa kwa WFP rasilimali zaidi zinazohitajika ili kurejesha usaidizi wa kawaida kwa wakimbizi barani Afrika kulingana na mahitaji yao ya chakula.”

Misaada ya chakula imepunguzwa kwa hadi asilimia 60 kwa wakimbizi wa Chad, huku wale wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini wakipokea nusu tu ya misaada ya chakula wanachohitaji.