Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ombi jipya la ufadhili kwa Ebola lazinduliwa kwenye jukwaa la Uchumi, Davos

Ombi jipya la ufadhili kwa Ebola lazinduliwa kwenye jukwaa la Uchumi, Davos

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Ebola, David Nabarro na Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu, Valerie Amos, leo wametoa ombi jipya la ufadhili kwa ajili ya kupambana na Ebola kwenye jukwaa la uchumi duniani huko Davos.

Ombi hilo ni la fedha zitakazosaidia juhudi za serikali za nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone, za kuwatambua na kuwatibu watu walioambukizwa kirusi cha Ebola, kuhakikisha mlipuko huo unakomeshwa haraka, kukwamua huduma muhimu za kijamii na kuboresha usalama wa chakula na lishe kwa watu.

Ombi hilo pia linajumuisha fedha zinazohitajika kuziwezesha nchi jirani kupunguza hatari za raia wao kuambukizwa kirusi cha Ebola.

Mahitaji ya kifedha kwa miezi sita ya kwanza ya mwaka 2015 kwa ajili ya Ebola ni dila bilioni 1.5. Tayari zimepatikana takriban dola milioni 500, na ombi hili linatarajiwa kujazia pengo lililopo la dola bilioni moja.