Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia za mwanga zinaweza kuboresha hali ya maisha- Ban

Teknolojia za mwanga zinaweza kuboresha hali ya maisha- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema leo kuwa teknolojia za mwangaza zinaweza kusaidia kupatia suluhu stahiki kwa changamoto nyingi, wakati huu ambapo dunia inajizatiti kutokomeza umaskini na kuendeleza utajiri jumuishi.

Kauli hiyo ya Bwana Ban ni sehemu ya maadhimisho kutangazwa mwaka huu wa 2015 kuwa mwaka wa mwangaza. Ban amesema teknolojia za mwangaza zitakuwa muhimu hata zaidi katika kuendeleza juhudi za kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia, kufikia malengo ya maendeleo endelevu siku zijazo, na pia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu amesema, kama sehemu ya juhudi za kueneza uwepo wa mwangaza, mkakati wake wa nishati endelevu kwa wote unalenga kuongeza upatikanaji wa nishati, matumizi bora ya nishati na matumizi ya nishati huishi ifikapo mwaka 2030. Hili litamaanisha mwangaza zaidi nyumbani, hospitalini na kwenye biashara- hali itakayochangia mustakhabali salama zaidi, wenye afya zaidi na wenye uzalishaji zaidi.