Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azindua maadhimisho ya miaka 70 ya UM

Ban azindua maadhimisho ya miaka 70 ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akiwa ziarani nchini India, amezindua maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa yatakayofikia kilele chake baadaye mwaka huu.

Akizungumza kwenye hafla hiyo mjini New Delhi, iliyomjumuisha pia mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Kailash Satyarthi na mabalozi wema wa Umoja wa Mataifa, Ban amesema uzinduzi huo ni fursa siyo tu ya kuazimia dunia pawe pahala pema kwa wote bali pia kujadili mustakhbali unaotakiwa.

Ametaja mambo makuu matatu yanayopaswa kuzingatiwa kuwa ni kuwekeza kwa wanawake na watoto ili kupata maendeleo duniani, kuhakikisha usawa miongoni mwa watu wote bila kujali tofauti zao na tatu kuimarisha ubia kati ya Umoja wa Mataifa na India kwani kwa kufanya hivyo siyo tu India inaimarika bali pia ulimwengu wote kwa ujumla.

Ban amerejelea kauli yake kuwa Umoja wa Mataifa ulio thabiti utamaanisha dunia bora zaidi na yenye amani.