Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ibn Chambas alaani jaribio la Mapinduzi Gambia

Ibn Chambas alaani jaribio la Mapinduzi Gambia

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Afrika Magharibi na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika Magharibi, UNOWA, Bw Mohammed Ibn Chambas, amelaani jaribio la hivi karibuni la kuchukua hatamu za uongozi kupitia kwa njia iliyo kinyume na kikatiba huko Gambia.

Katika taarifa Ibn Chambas amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa ambao jukumu lake la kimsingi ni amani na usalama, hautakubali majaribio yatakayovuruga utaratibu wa kikatiba.

Halikadhalika, Ibn Chambas amekariri sera ya Umoja wa Afrika na jumuiya nchi za Afrika Magharibi ya kutovumilia mapinduzi ya serikali barani Africa.

Aidha, Mwakilishi huyo maalum anayetarajia kutembelea Gambia, na kusihi mamlaka nchini humo, haswa vikosi vya ulinzi kuhakikisha uchunguzi unafanyika katika mukhtadha wa heshima kamili ya haki za binadamu na mchakato wa kisheria.