Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataja ya kuzingatia 2015, asifu tangazo la Marekani kuhusu Cuba

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akizungumza na waandishi wa habari (Picha:Maktaba)

Ban ataja ya kuzingatia 2015, asifu tangazo la Marekani kuhusu Cuba

Mwaka wa 2015 ni lazima uwe wa kuchukua hatua duniani ili kupunguza machungu yanayokabili wakazi wa dunia kutokana na majanga ya kiasili na yale yanayosababishwa na binadamu ikiwemo mapigano.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York, ikiwa ni mkutano wake wa mwisho wa mwaka akitaja mambo manne makuu yanayopaswa kupatiwa kipaumbele mwakani kwa kuzingatia matumaini na machungu yaliyoshuhudiwa mwaka huu wa 2014.

Mambo hayo ni pamoja na dunia kuwa na matumaini ya kuwa na makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi, pili kumaliza jinamizi la mzozo wa Syria ili kudhibiti kuzidi kuzorota kwa usalama na tatu..

(Sauti ya Ban)

“Tuchukue hatua Zaidi kudhibiti misimamo mikali na ongezeko la vyama vya kisiasa vyenye misimamo mikali ambavyo vinalenga makundi madogo na hususan waislamu. Nne Umoja wa Mataifa utaendelea kutekeleza majukumu yake kulingana na mabadiliko mapya duniani.”

Ban amegusia pia tathmini muhimu za majukumu ya Umoja wa Mataifa zinazofanyika sasa ikiwemo ulinzi na ujenzi wa amani akisema zitakamilishwa mwakani..

(Sauti ya Ban)

“Tathmini hizi ni fursa za kuendeleza marekebisho mengine ambayo yameanza katika kipindi chote cha utendaji wangu”

Katibu Mkuu akaulizwa msimamo wa Umoja wa Mataifa kufuatia tangazo la Marekani kuhusu kurejesha uhusiano wake na Cuba uliokuwa na umedorora tangu miaka ya 1960.

(Sauti ya Ban)

“Habari hii ni nzuri sana, napenda kuwapongeza Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Raul Castro wa Cuba kwa kuchukua hatua hii muhimu ya kuelekea kurejesha katika hali nzuri uhusiano kati ya nchi zao. Kadri ambavyo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimekuwa zikisisitiza kupitia maazimio ya Baraza Kuu kwa miaka kadhaa, wakati umefika kwa Cuba na Marekani kurejesha uhusiano kati yao. Ni matumaini yangu ya dhati kuwa tangazo hili litasaidia kupanua zaidi uhusiano kati ya wananchi wa nchi mbili hizo ambao wametenganishwa kwa kipindi kirefu.”

Jioni ya leo Katibu Mkuu anaelekea Afrika Magharibi ambako atatembelea nchi nne zilizokumbwa zaidi na Ebola ambazo ni Guinea, Liberia, Mali na Sierra Leone ili kujionea hali halisi ya maambukizi na hatua zinazochukuliwa kudhibiti ugonjwa huo. halikadhalika atakwenda Ghana ambako ndio makao makuu ya Ofisi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaohusika na dharura ya Ebola, UNMEER.