Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Munich umeleta mabadiliko makubwa ya ulinzi duniani: Ban

Mkutano wa Munich umeleta mabadiliko makubwa ya ulinzi duniani: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ambaye yuko ziarani huko Ulaya amezungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya mkutano wa kimataifa wa usalama wa Munich huko Ujerumani na kusema kuwa mkutano huo katika miongo mitano ya uwepo wake umeweka historia.

Mathalani amesema miaka 25 ya kwanza uliweza kuvunja kuta kati ya watu na itikadi na robo ya pili umekuwa mstari wa mbele kuendeleza fikra mpya za ulinzi duniani.

Amesema mabadiliko ya sasa ya teknolojia yanaleta mambo ya kisasa ya manufaa na wakati huo huo kuweka jamii nyingine hatarini zaidi na hivyo mwelekeo mpya unahitajika kuondoa tofauti hizo.

Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa unaibuka kukabiliana na changamoto hizo kwa njia ya mashauriano, diplomasia, ulinzi na ujenzi wa Amani lakini kupitia mkutano wa Munich dunia inaweza kubaini mbinu za kisasa za kuweka ulinzi ambao kila mtu anahitaji na dunia ina uwezo wa kumpatia.

Katibu Mkuu ametolea mfano wa mizozo inayoendelea huko Syria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na hata Sudan Kusini akisema kuwa kuna umuhimu wa kulinda raia dhidi ya ukiukwaji mkubwa wa haki.

Amesema ni matumani ya yake kuwa viongozi wa Afrika wanaokutana Addis Ababa, Ethiopia wataonyesha uungaji mkono wa majeshi ya Afrika yanayolinda amani sehemu mbali mbali barani humo.