Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kifuta jasho kwa wafanyakazi wa Ebola kulipwa kupitia simu ya mkononi

Picha: ITU/V. Martin

Kifuta jasho kwa wafanyakazi wa Ebola kulipwa kupitia simu ya mkononi

Kwa mara ya kwanza nchini Sierra Leone, malipo ya fidia au kifuta jasho kwa kwa wafanyakazi wanaohusika na harakati dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola yatafanyika kupitia simu za mkononi.

Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo, UNDP nchini humo Sudipto Mukerjee amesema hatua hiyo ni muhimu kwani itatoa hakikisho la malipo yao kwa wakati na upatikanaji wa watoa huduma.

Mukerjee amesema wafanyakazi hao wako mstari wa mbele na wanaweza kuwa hai leo na kesho yake wakafariki dunia na iwapo hawapati fedha zao kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa wanakata tamaa na wanagoma kufanya kazi ikimaanisha vita dhidi ya Ebola inakumbwa na mkwamo.

UNDP inasema changamoto kubwa kudhibiti Ebola ni rasilimali ya watu akisema unaweza kutumia muda mchache kujenga kituo cha matibabu au cha huduma za jamii lakini kupata wahudumu wenye sifa kusimamia vituo hivyo ni changamoto kubwa.

Mfumo huo wa malipo umebuniwa kwa ushirikiano baina ya UNMEER na mashirika ya binafsi kama vile Airtel, Africel and Splash money.