Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano kati ya UM na AU kwenye amani waangaziwa

Picha: UNAMID

Ushirikiano kati ya UM na AU kwenye amani waangaziwa

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala kuhusu operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa zinazofanyika kwa ushirikiano na Muungano wa Afrika. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Katika mjadala huo Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili ni muhimu kwa ajili ya kulinda amani akisema ni vyema ushirikiano huo ukawa wa kimkakati zaidi ili kuweza kuzuia mizozo, kuishughulikia na kuitatua mizozo.

Amesema ni kwa mantiki hiyo ameanzisha tathmini ya ushirikiano huo ambao ripoti yake itawekwa wazi mwezi Machi licha ya mafanikio yaliyopatikana maeneo mbali mbali akitolea mfano Somalia ambako wanashirikiana na IGAD kusaidia uimarishaji wa serikali kuu.

(Sauti ya Ban)

“Wakati umefika kusogeza ubia wetu kwenye kiwango cha uwazi, uweze kutekelezeka na uhakika. Baraza linaelewa fika kuwa mizozo ya Afrika siyo ya Afrika pekee bali inahusisha jamii nzima ya kimataifa na itaweza kutatuliwa pale tu jamii hiyo itakapokuwa kitu kimoja.”

Mwingine aliyehutubia baraza ni Mkuu wa Muungano wa Afrika huko Mali na ukanda wa Sahel, Pierre Buyoya ambaye amesema ushirikiano kati yao na Umoja wa Mataifa ni wa kipekee..

(Sauti ya Buyoya)

"Ushirikiano huo wa kimkakati umewezesha taasisi zetu mbili kuanzisha mijadala ya mara kwa mara kuhusu maswala yanayotuhusu sisi sote juu ya mambo ya amani na usalama, ambapo ushirikiano wetu umekuwa zaidi na umeonekana zaidi. "