Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikoko ina nafasi kubwa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi:UNEP

Picha: UNEP

Mikoko ina nafasi kubwa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi:UNEP

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na mazingira, UNEP imesema mikoko ina nafasi kubwa ya kufyonza hewa ya ukaa kuliko miti iliyoko kwenye misitu ya kawaida lakini bado haitumiki ipasavyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo huko Lima, Peru kando ya mkutano wa 20 wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Achim Steiner amesema badala yake mikoko hivi sasa inakatwa kwa kasi isiyo ya kawaida.

Amesema gharama ya uharibifu wa mikoko kwa mwaka ni dola bilioni 42 na hivyo ripoti imetaka watunga sera kuchukua hatua kulinda miti hiyo na kujumuisha kwenye mkakati wa kupunguza uchafuzi utokanao na uharibifu wa Misitu, REDD.

Mkuu huyo wa UNEP amesema udhibiti wa maeneo oevu ikiwemo yale ya pwani ni jambo bora akitolea mfano miradi ya huko Kenya, Senegal kuwa inaanza kuleta mafanikio ya uhifadhi wa mazingira ikiwemo kupunguza ukataji haramu wa mikoko.