WFP yaahirisha mgao wa chakula kwa wakimbizi wa Syria
Mgogoro wa kifedha unalilazimu shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP kuahirisha mgawo wa vocha za chakula kwa wakimbizi wa Syria zaidi ya milioni moja na laki saba.
Wakimbizi wa Syria walionufaika kupitia mradi huo ni wale waliokimbilia nchini Jordan, Lebanon, Turkey, Iraq na Misri ambao wamekuwa wakitumia vocha hizo kununua vyakula katika maduka.
WFP imeonya kuwa bila vocha hizo familia nyingi zitakumbwa na njaa.
Madhara ya kusitishwa kwa msaada huo ambayo yameelezwa kama janga na mkuu wa WFP Ertharin Cousin hususani kwa wakimbizi ambao wanapambana kukabiliana na msimu wa baridi kali.
Amesema mashirika mengi ya dharura ya operesheni huko Syria yako katika wakati mgumu kifedha yakisaka huduma hiyo huku ahadi nyingi za wahisani zikiwa hazijatekelezwa.
WFP inahitaji kiasi cha dola za kimarekani milioni 64 kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Syria waliokimbilia nchi jirani, kiwango hicho kikiwa kwa ajili ya mwezi December pekee.