Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani shambulizi la bomu Yobe, Nigeria

Ban alaani shambulizi la bomu Yobe, Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani vikali shambulizi la bomu lililotekelezwa leo dhidi ya shule moja ya malazi huko Potiskum, Kaskazini Mashariki mwa jimbo la Yobe, Nigeria, na ambalo limeripotiwa kuwaua wanafunzi kadhaa na kuwajeruhi wengine wengi.

Katibu Mkuu ametoa wito waliutekeleza uhalifu huo wafikishwe mara moja mbele ya mkono wa sheria katika utaratibu unaoheshimu wajibu wa Nigeria kuhusu haki za binadamu, na hatua zichukuliwe kutoa ulinzi kwa raia ipasavyo.

Katibu Mkuu amepeleka rambi rambi zake kwa familia za wahanga, serikali na watu wa Nigeria. Taarifa ya msemaji wake imesema Katibu Mkuu ameghadhabishwa na mashambulizi na ukatili wa mara kwa mara dhidi ya taasisi za elimu kasakazini mwa nchi hiyo, na amekariri wito wake wa kukomeshwa mara moja uhalifu huu wa kinyama.

Shirika la Kuhudumia Watoto UNICEF, pia limetoa taarifa ya kulaani mashambulizi dhidi ya watoto na shule, kwa mujibu wa msemaji wa Katibu Mkuu, Farhan Haq...

“UNICEF imesema mashambulizi haya ya mara kwa mara dhidi ya watoto na shule ni mashambulizi kwa mustakhbali wa Nigeria, taifa ambalo tayari ndilo lililo na idadi kubwa zaidi ya watoto wasio shuleni duniani. UNICEF imetoa wito kwa wenye wajibu na uwezo kuwafikisha wahalifu mbele ya sharia, na kutimiza wajibu wa kuwalinda watoto.”