Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahitaji zaidi yatakiwa huko CAR; Ni pamoja na chanjo

Picha: OCHA/Gemma Cortes

Mahitaji zaidi yatakiwa huko CAR; Ni pamoja na chanjo

Mratibu Mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Claire Bourgeois, ametembelea kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo na kubaini kuwa wakazi wa jimbo la Vikaga wanahitaji misaada zaidi ya haraka.

Katika ziara hiyo aliambatana na wawakilishi wa Wizara ya masuala ya kibinadamu, mashirika ya kimataifa na yasiyo ya kiserikali ambapo wamejionea hali halisi ya uhitaji wa chakula, mahitaji ya afya na elimu.

Mathalani kuhusu afya jambo la chanjo lilijitokeza ambapo Bi. Bourgeois amesema haikubaliki kusikia kwamba zoezi la kawaida la chanjo haliwezi kuendelea kwa sababu majokofu yamechelewa kufika au kwa sababu ya ukosefu wa usalama barabarani.

Alikutana pia na watu waliokimbia maeneo ya kijijini kutoka mji mkuu Bangui na ambao sasa wana hofu ya kurejea makwao.