Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa dunia waanza ziara ya kihistoria Pembe ya Afrika

UN Photo/Tobin Jones)
Picha:

Viongozi wa dunia waanza ziara ya kihistoria Pembe ya Afrika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na viongozi wengine wa dunia, leo wameanza ziara ya kihistoria katika eneo hilo na kuelezea namna walivyo tayari kutoa uungaji mkono wa kisiasa na usaidizi mkubwa wa kifedha kwa nchi za Pembe ya Afrika. Taarifa kamili na Abdullahi Boru.

(Taarifa ya Abdullahi Boru)

Viongozi wa dunia pamoja na watendaji wakuu wa taasisi za kikanda leo wameanza ziara ya kihistoria katika eneo la Pembe ya Afrika ambako wataelezea namna walivyo tayari kuiunga mkono michakato ya kisiasa katika eneo hilo.

Watendaji hao wanatarajia kuongeza msukumo mpya wa kulisaidia eneo hilo ambalo linakabiliwa na hali ngumu kwa kutoa ahadi ya michango ya fedha.

Katika siku ya kwanza ya safari hiyo, benki ya dunia imetangaza kulipiga jeki eneo hilo akiahidi kutenga kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.8 kiwango ambacho kitatumika kuimarisha miradi mbalimbali ikiwemo ile ya ukuzaji uchumi.

Mpango huo ambao unalenga kukabiliana na tatizo la umaskini na ukuzaji ajira utazilenga nchi nane za Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na  Uganda.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeongoza ujumbe huo alisifu juhudi zinazochukuliwa na nchi zilizoko katika Pembe ya Afrika ambazo alisema kuwa zimepiga hatua kwa kujenga uchumi imara na wenye kutoa tija.

Alisema kuwa kwa kutambua hilo, Umoja wa Mataifa unaungana na taasisi nyingine duniani kuunga mkono juhudi hizo na kwamba hatua kubwa inayozingatiwa sasa ni kuhakikisha kwamba eneo hilo linakuwa na amani ya kudumu.