Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMEER yaweka mpango kabambe wa kusaidia nchi zilizoathiriwa na Ebola

Mkuu wa UNMEER Anthony Banbury. (Picha:UN/Eskinder Debebe)

UNMEER yaweka mpango kabambe wa kusaidia nchi zilizoathiriwa na Ebola

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuchukua hatua za dharura dhidi ya Ebola, UNMEER, Anthony Banbury, amekamilisha msururu wa mashauriano na marais wa Guinea, Liberia na Sierra Leone kuhusu usaidizi wa jamii ya kimataifa katika juhudi za kupambana na tatizo la Ebola.

Mnamo Ijumaa, Bwana Banbury alikutana na Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, baada ya kukutana na marais Alpha Conde wa Guinea, na Ernest Bai Koroma wa Sierra Leone mwanzoni mwa wiki. Mbali na viongozi hao, alikutana pia na wadau mbalimbali na kuzuru vituo vya afya vinavyojengwa ili kusikia na kujionea jinsi juhudi za kukomesha kuenea kwa kirusi cha Ebola zinavyoendelea.

Mazungumzo na viongozi wa nchi zilizoathiriwa yaliangazia jinsi mkakati wa usaidizi wa kimataifa unavyoweza kuwekwa na kutekelezwa ili kusaidia juhudi zinazoendelea za kitaifa. Mkakati huo ambao ulibuniwa wiki iliyopita, utakuwa mwongozo wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhusu ufadhili na mipango yote.