Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanachama wapya wasio wa kudumu wachaguliwa kwa Baraza la Usalama

UN Photo/Amanda Voisard
Picha:

Wanachama wapya wasio wa kudumu wachaguliwa kwa Baraza la Usalama

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, leo limefanya uchaguzi wa wanachama wasio wa kudumu katika Baraza la Usalama, ambao watahudumu kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari mwakani. Hapa, ni Rais wa Baraza Kuu Sam Kutesa, akitangaza matokeo ya kura pekee iliyopigwa.

“Baada ya kupata thuluthi mbili za wingi wa kura zinazohitajika, Uhispania imechaguliwa kuwa mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari mosi 2015.”

Uhispania imeipiku Uturuki kuuwakilisha ukanda wa Ulaya Magharibi na nchi nyingine, kwa kupata kura 132.

Nchi nyingine ambazo zimechaguliwa kuwa wanachama wa Baraza la Usalama kwa kipindi hicho kuanzia Januari 2015, ni Angola, Malaysia, New Zealand na Venezuela.

Nchi ambazo muda wao wa uanachama unakamilika mwishoni mwa mwaka huu ni Argentina, Australia, Luxembourg, Jamhuri ya Korea (Kusini) na Rwanda.

Wanachama wengine wasio wa Kudumu katika Baraza la Usalama watakaohudumu mwaka 2015 ni Chad, Chile, Jordan, Lithuania na Nigeria. Rais wa Baraza Kuu ameeleza zaidi

“Miongoni mwa wanachama wasio wa kudumu, watakaobaki ofisini mwaka 2015, watatu wanatoka Afrika na Asia Pasifiki, mmoja kutoka Ulaya Mashariki, na mmoja kutoka nchi za Amerika ya Kusini na eneo la Karibe.”

Kwa nafasi mbili za Afrika na Asia na Pasifiki, Angola na Malaysia zilipita bila kupingwa, huku Venezuela ikipita bila kupingwa kuuwakilisha ukanda wa Amerika ya Kusini na Karibe.

Wanachama wa Kudumu wa Baraza la Usalama ni Marekani, Uchina, Ufaransa, Uigereza na Urusi, na wana mamlaka ya kura ya turufu.