Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola na ISIL havikuibuka kama uyoga: Kamishna Zeid

UN Photo - Jean-Marc Ferre
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein. Picha:

Ebola na ISIL havikuibuka kama uyoga: Kamishna Zeid

Kamishna mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra'ad Al Hussein amesema hali iliyofikia sasa ya Ebola na ISIL ni matokeo ya kupuuzwa kwa majanga hayo pindi yalipoanza kuibuka taratibu. Amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva kama anavyoripoti Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Zeid Ra’ad Al Hussein amesema jamii ya kimataifa ilishindwa kutambua mapema athari za majanga hayo mawili mlipuko wa Ebola ni matokeo ya kupuuzwa kwa haki za binadamu pindi hatua mbali mbali zinapotekelezwa na sasa kinachodhihirika ni ukosefu wa misingi hiyo.

Amesema ofisi yake inaandaa miongozo ili hata karantini zinazowekwa dhidi ya wagonjwa zisikiuke haki za binadamu huku akitoa angalizo.

(Sauti ya Zeid)

“Uwezo wa Ebola kuteketeza maisha ya binadamu kwa kiwango kikubwa sasa ni dhahiri. Uwezo wake wa kukandamiza haki za binadamu za wale waliopona bado haujazingatiwa. Kupatia umuhimu mdogo haki za binadamu hasa ile ya afya, elimu, usafi wa mazingira, maendeleo na utawala bora ndio chanzo cha mlipuko huu na hadi sasa hakijajadiliwa.”

Kamishna Zeid akatanabaisha kuhusu kikundi cha ISIL.

(Sauti ya Kamishna Zeid)

“Lakini ISIL, kama Ebola, haikuanza ghafla. ISIL iliweza kuenea kwa hila na baada ya kushika kasi ya kutosha ikaibuka kama dhoruba kutoka Iraq kwenda Syria na kurejea Iraq. Na ikaweza kuingia kwenye kaya zetu kupitia kamera na kompyuta zao kwenye mitandao ya kijamii.”