MINUSMA imekuwa mlengwa wa wanamgambo Mali: Ladsous

8 Oktoba 2014

Baraza la usalama leo limekutana kuhusu hali ya Mali, mkuu wa Idara ya operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Herve Ladsous akiwaelezea wanachama wa baraza hilo wasiwasi wake kuhusu hali ya usalama.

Amesema mashambulizi dhidi ya walinda amani yameongezeka sana tangu kujitoa kwa jeshi la serikali la Mali na jeshi la Ufaransa kwenye maeneo ya kaskazini mwa Mali.

(Sauti ya Ladsous)

Kwa kweli, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa MINUSMA umebaki ujumbe wa kimataifa na wa kigeni pekee kwenye eneo hilo. Kwa hiyo tumekuwa walengwa wa kwanza kutoka kwa waharibifu, watu wenye msimamo mkali, majihadi, wafanyabishara wa magendo na wote ambao wangetaka kutawala eneo hilo pekee yao ili waendelee na shughuli zao zisizo za kimaadili.”

Amesema jumla ya walinda amani 31 wameuawa na wengine 91 wamejeruhiwa tangu Julai 2013 nchini Mali. Ladsous amesikitishwa na mauaji wa walinda amani wa Chad, Niger na Senegal yaliyotokea kwa kipindi cha siku chache zilizopita, akisema idadi ya vifo vya walinda amani Mali ni kubwa kuliko operesheni zote zingine za Umoja wa Mataifa.

Ameomba ushirikiano wa wadau wote katika kurejesha hali ya usalama kwenye maeneo hayo, akitoa wito pia kwa pande za mzozo kufikisha haraka makubaliano ya kisiasa.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani vikali mauaji ya mlinda amani mmoja wa Senegal yaliyotokea tarehe 7 Oktoba karibu ya kambi ya MINUSMA.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter