Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabilioni ya fedha yatapotea iwapo ongezeko la asidi baharini halitasitishwa- UM

UN Photo/Stuart Price
Bahari. Picha@

Mabilioni ya fedha yatapotea iwapo ongezeko la asidi baharini halitasitishwa- UM

Uchumi wa kimataifa utapoteza mabilioni ya fedha iwapo hatua hazitachukuliwa kukomesha ongezeko la aside baharini, imeonya ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa, ambayo imezinduliwa leo katika mji wa Pyeongchang katika Jamhuri ya Korea Kusini, wakati wa mkutano wa 12 wa Mkataba kuhusu Bayo-anuai, COP-12.

Inakadiriwa kuwa uchumi wa kaimataifa huenda ukapoteza takriban dola trilioni 1 kila mwaka ifikapo mwisho wa karne hii iwapo nchi hazitachukua hizo hatua stahili.

Kiasi hicho cha fedha kinaonyesha hasara ya kiuchumi ambayo zitapata sekta zinazotegemea miamba ya matumbawe pekee, ambayo inadhaniwa kuhatarishwa zaidi. Hata hivyo, hasara kamili ya kimazingira kwa ujumla haijulikani.

Mratibu wa masuala na sera kuhusu Bayo-anuai katikka Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, Salvatore Arico, amesema kuwa iwapo mifumo-mazingira kama miamba ya matumbwe itaathiriwa na isichangie kama inavyochangia sasa, hali ya maisha ya watu wanaoitegemea itaathiriwa.