Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili hali ya Gaza

UN Photo.
Baraza la Usalama.

Baraza la Usalama lajadili hali ya Gaza

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana leo kujadili hali Gaza, ambapo pia limehutubiwa na Mratibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu harakati za amani Gaza, Robert Serry.

Bwana Serry ametoa taarifa kwa Baraza hilo kuhusu kazi ya Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono utekelezaji wa makubaliano ya usitishwaji mapigano Gaza, pamoja na kazi ya Umoja wa Mataifa Syria.

Bwana Serry amesema kinachohitajika kuepukana na kile kilichosababisha mzozo wa hivi karibuni sasa kimeanza kushughulikiwa. Ametangaza kuwa Umoja wa Mataifa umefikia maafikiano na mamlaka za Palestina Ramallah na serikali ya Israel kuhusu mkakati mpya wa ukarabati wa muda. Amewaelezea waandishi wa habari kuhusu mkakati huo

“Ukitekelezwa vyema na pande zote husika, mkakati huo utatuwezesha kuanza haraka iwezekanavyo ukwamuaji na ukarabati unaohitajika mno Gaza, na kwa hiyo tutahitaji vifaa vya ujenzi kwa wingi na vitu vinginevyo ambavyo Israel imeorodhesha.”

Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Baraza la Usalama, Samantha Power ndiye rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu, na amewahutubia pia waandishi wa habari muda mfupi baada ya Bwana Serry.

“Mazungumzo yetu pia yalimulika Iraq, na wanachama wa Baraza waliuliza maswali kadhaa kuhusu masuala haya yote. Kuhusu Gaza, wanachama wa Baraza walijadili usitishwaji mapigano, ambao unaendelea kutekelezwa, pamoja na ufikishaji misaada ya kibinadamu na juhudi za ukarabati kupitia njia mpya iliyokubaliwa. Kuhusu Syria, wanachama wa Baraza wameelezea uungaji mkono wao kwa mjumbe maalum de Mistura, na ujumbe wake. Wanachama wa Baraza wanaendelea kuamini kuwa suluhu pekee kwa mzozo huo ni ya kisiasa.”