Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pazia lafungwa rasmi mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la UM

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa John Ashe akihutubia kwa mara ya mwisho baraza hilo. (Picha:UN /Eskinder Debebe)

Pazia lafungwa rasmi mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la UM

Hatimaye mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umefikia rasmi ukomo wake Jumatatu ya tarehe 15 Septamba mwaka 2014 na kuashiria kuanza kwa mkutano wa 69.

Akizungumza kwenye hitimisho la mkutano huo, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema mkutano ulikuwa na manufaa na umeweka msingi wa mjadala muhimu kwa mustakhbali wa dunia kuanzia maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015 na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Bwana Ban pamoja na kumpongeza Rais wa BarazahiloJohn Ashe akaenda mbali zaidi akisema..

“Huu umekuwa ni mwaka wa matukio mengi! Tulianza na ajenda kamili yenye majukumu. Lakini pia tulikumbana na majanga mbali mbali duniani ambayo yalidororesha Baraza la Usalama, huku Baraza Kuu likiibuka na kuchukua hatua.”

Rais wa Baraza anayemaliza muda wake John Ashe alishukuru wajumbe kwa kushiriki kikamilifu katika lengo lake la kuhakikisha anaweka mazingira muafaka ya mjadala wa ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015.  Hata hivyo akataka wasionee haya hoja ya marejebisho ya baraza la usalama.

“Wakati itakuwa ni ukosefu wa busara kupuuzia changamoto zilizojikita kwenye mjadala halisi wa marekebisho ya baraza la usalama, bado haipaswi kuwa sababu ya kutufanya kuondokana na hoja hiyo. Iwapo tunapaswa kuwa na taasisi yenye uwakilishi wa dhati na inayodhihirisha uanachama wa sasa tofauti na miongo iliyopita, ni lazima sasa na si baadaye tusake mbinu ya kufanya hivyo.”

Shughuli hii iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza Kuu uliokarabatiwa tayari kwa mkutano wa 69 ilihudhuriwa na Rais wa mkutano huo wa 69 Sam Kutesa.